Ngoma nzito, Jaji Mkuu apingwa kortini

Welcome to our community

Looks like you don't have an account yet? Be apart of something great, join today! Create account to get more access like posting, reacting to others helpful post and your own private message Register Or Login

Gily

KF Founder & Dragon IGM
Staff member
Jun 4, 2023
7,020
22,618
113
Dar es Salaam. Sakata la Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Juma kuongezewa muda wa utumishi wa wadhifa huo sasa limetinga mahakamani baada ya wakili mmoja kufungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu Masjala Kuu, akipinga hatua hiyo.

Wakili huyo, Humphrey Malenga amefungua kesi hiyo siku chache baada ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Stella Mugasha kumwandikia barua Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel akikosoa uamuzi huo wa Rais Samia Suluhu Hassan akisema ni uvunjaji wa Katiba.

Hii ni kesi ya kihistoria kufunguliwa mahakamani ya kupinga Jaji Mkuu kuongezewa na Rais muda wa utumishi.

Profesa Juma aliyezaliwa Juni 15, 1958 amekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania kwa miaka mitano na miezi tisa kuanzia Septemba 10, 2017, alimaliza utumishi wake kwa nafasi hiyo Juni 15, 2023 baada ya kufikisha umri wa miaka 65, kwa mujibu wa Katiba.

Hata hivyo, Rais Samia anadaiwa kumwongezea muda wa kuendelea na utumishi katika nafasi hiyo kwa muda ambao bado haujawekwa wazi.
Taarifa za Rais kumwongezea muda Profesa Juma ziliianza kusambaa na kuibua mjadala baada ya kuvuja kwa barua hiyo ya Jaji Mugasha katika mitandao ya kijamii.

Katika barua hiyo Jaji Mugasha ambaye alilithibitishia Mwananchi kuandika barua hiyo, anasema uamuzi huo ni ukiukwaji wa Katiba na kutozingatia misingi ya sheria.

Nakala ya barua hiyo ya kurasa kumi ilitumwa pia kwa Rais Samia, Profesa Juma, Jaji wa Rufani, Augustine Mwarija, Jaji Kiongozi, Mustapher Siyani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Eliezer Feleshi na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk Moses Kusiluka

Katika shauri hilo dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Malenga anaiomba Mahakama Kuu itoe tafsiri ya ibara za Katiba kuhusu mamlaka ya Rais kuahirisha au kuongeza umri wa kustaafu wa utumishi wa Jaji Mkuu.

Ibara hizo ambazo Malenga anaiomba mahakama hiyo izitolee tafsiri ni ibara ya 118(2) na 120 (2) na (3).

Ibara ya 118(2) inaeleza kuwa Jaji Mkuu ambaye ni mkuu wa Mahakama ya Rufani na Mhimili wa Mahakama kwa ujumla atatumikia wadhifa huo mpaka atakapotimiza umri wa kustaafu wa Jaji wa Mahakama ya Rufani.

Ibara ya 120 (2) na (3) zinabainisha kuwa umri wa kustaafu wa Jaji wa Mahakama wa Rufani ni miaka 65, lakini inabainisha kuwa Rais akiona inafaa anaweza kumuongezea muda maalumu mpaka mwisho wa muda huo wa nyongeza utakapoisha.

Ibara 120(4) inafafanua kuwa pia Jaji wa Mahakama ya Rufani anaweza kuendelea na majukumu yake hata baada ya kufikisha umri wa miaka 65 hadi pale atakapokamilisha kuandaa na kutoa hukumu za mashauri ya kesi alizozisikiliza au shughuli au mashauri aliyokwishaanza kuyasikiliza.

Mjadala unaoibuka hapa ni kama masharti ya ibara 120(2) (3) kuhusu jaji wa Mahakama ya Rufani kuongezewa muda wa utumishi zinasomwa pamoja na ibara ya 118(2), ili kumaanisha kwamba masharti hayo yanamhusu pia Jaji Mkuu.

Kwa mujibu wa Jaji Mugasha, Ibara ya 118(2) inayohusu umri wa kustaafu wa Jaji Mkuu, ambao ni sawa na wa jaji mwingine wa kawaida wa Mahakama ya Rufani (miaka 65), inasimama pekee yake na wala haihusiani na ibara ya 120(2) na (3).

Hivyo, Malenga anaiomba mahakama hiyo itoe tafsiri ya masharti ya Ibara ya 118(2) kuhusu umri wa kustaafu wa Jaji Mkuu, kwamba ni miaka 65 na si umri wa kustaafu wa jaji wa kawaida wa Mahakama ya Rufani.

Anaiomba pia mahakama hiyo itoe tafsiri kwamba Ibara ya 118(2) ni ibara inayosimama peke yake, haihusiani na Ibara ya 120(1), (2), (3) na (4) katika kuamua umri wa kustaafu utumishi wa Jaji Mkuu.

Vilevile Malenga anaiomba mahakama itafsiri kwamba mamlaka ya Rais kuzuia kustaafu au kumuongezea muda wa utumishi Jaji wa Mahakama ya Rufani kwa masilahi ya umma kwa mujibu wa ibara hiyo ya 120(2) na (3), hayatumiki kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Jaji Mkuu.

Mwisho, anaiomba mahakama hiyo itamke kwamba kuahirishwa kwa uamuzi wa kustaafu au kuongezewa muda wa utumishi wa Jaji wa Mahakama ya Rufani wa sasa, ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Juma kwa mujibu wa Ibara ya 120(2) na au 120(3), ni kinyume cha Katiba.
Kesi hiyo ilifunguliwa mahakamani hapo Juni 28, mwaka huu imepangwa kusikilizwa na Jaji Godfrey Isaya na ilitajwa kwa mara ya kwanza jana mbele ya mawakili wa pande zote.

Malenga anawakilishwa na jopo la mawakili watatu, Ipilinga Panya, Aliko Mwamanenge na Joyce Brown na Serikali iliwakilishwa na mawakili wa Serikali Alice Mturo na Bravoo Junus ambao waliomba na kuruhusiwa na mahakama kuwasilisha majibu ya Serikali ya maandishi Julai 6, mwaka huu.

Barua ya Jaji Stella
Jaji Mugasha katika barua yake alisema, “kila Jaji wa Mahakama ya Rufani atalazimika kuacha kazi yake atakapotimiza umri wa miaka 65, lakini masharti ya ibara hii ndogo yatatumika bila kuathiri masharti yafuatayo katika ibara hii”.

Hata hivyo, uamuzi wa Rais Samia ni kwa mujibu wa Ibara ya 120 (3) ya Katiba ya Tanzania, inayompa mamlaka mkuu wa nchi kumwongezea muda Jaji wa Mahakama ya Rufani hata akifikisha muda wa kustaafu, iwapo ataona kuna manufaa ya umma.
Kulingana na ibara hiyo, “iwapo Rais ataona kwa ajili ya manufaa ya umma inafaa Jaji wa Mahakama ya Rufani aliyetimiza umri wa miaka 65 aendelee kufanya kazi na huyo Jaji mwenyewe wa Mahakama ya Rufani atakubali kwa maandishi kuendelea kufanya kazi.

“Basi Rais aweza kuagiza kuwa Jaji huyo wa Mahakama ya Rufani aendelee kufanya kazi kwa muda wowote utakaotajwa na Rais.”

Jaji Stella alirejea mwaka 1995 na 2000, ambapo ibara ya II8 haikuwa na kipengele kinachoweka umri wa miaka 65 kuwa ni ukomo wa Jaji Mkuu kuhudumu katika nafasi hiyo.
“Mwaka 2005 kupitia Sheria ya Mabadiliko ya 14 katika Katiba, Sheria Na. 1 ya mwaka 2005, Ibara yote ya 118 ilifutwa na kutungwa upya. Mabadiliko hayo yaliridhiwa na Rais Aprili 6, 2005.

Ibara ya 118 (2) inaeleza, Jaji Mkuu atateuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa za kuwa Jaji wa Rufani na atakuwa ndiye Kiongozi wa Mahakama ya Rufani na pia Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kama ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 116 ya Katiba na atashika madaraka hadi atakapotimiza umri wa kustaafu kama Jaji wa Rufani, isipokuwa kama:
(a) atajiuzulu,​
(b) kiti chake kitakuwa wazi kutokana na maradhi au kifo,​
(c) atavuliwa wadhifa wa Jaji Mkuu na Rais,’’ aliandika.​

Jaji Stella alielezea kuwahi kuwepo mjadala ndani ya Mahakama kuhusu uhalali wa majaji waliotimiza umri wa kustaafu na kuongezewa muda wa kuhudumu ikiwa ni pamoja na Jaji Mkuu.
Wakati wa mjadala huo, Jaji Stella alieleza kuwa Jaji Mwarija alikuwa ni Msajili wa Mahakama ya Rufaa na Mtendaji wa Mahakama kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu Novemba, 2006.

Kutokana na mjadala huo, Agosti 6, 2007, Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa wakati huo, Johnson Mwanyika alimwandikia barua Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma akielezea utaratibu wa kuwaongezea ajira majaji baada ya kustaafu.

“Anayestahili kuongezewa muda ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, ilitamkwa wazi Jaji Mkuu anatakiwa kustaafu atimizapo umri wa miaka 65 na hastahili kuongezewa muda wowote au mkataba wa kuendelea kufanya kazi kama Jaji Mkuu,” inaeleza sehemu ya barua hiyo ambayo pia nakala yake ilitumwa kwa Jaji Mkuu wa wakati huo, Augustino Ramadhani na Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo.

Katika barua hiyo iliyolenga kuondoa utata wa muda wa kustaafu kwa jaji mkuu, alisema, “Rais ametoa mwongozo wa kushughulikia nyongeza ya muda wa kustaafu kama ifuatavyo: Nashauri njia itafutwe kuondoa migongano ya vifungu vya ukomo wa ajira ya mikataba.

“Ni vema iendelee kuwepo fursa hiyo.
Kwa Jaji Mkuu, naafiki pasiwepo na nyongeza ya utumishi na wala sioni haja ya kubaki (kama) Jaji wa Rufani wa kawaida, haipendezi,” aliandika Mwanasheria Mkuu Mwanyika wakati huo.

Baada ya Barua hiyo ya Mwanyika, Majaji wakuu waliofuatia walistaafu kwa umri wa miaka 65, mfano ni Jaji Mkuu Mstaafu, Chande Othman alipomaliza muda wake alistaafu na alionyesha wazi kwamba hakuwa na nia ya kuendelea hata angeongezewa muda,” alisema.

MWANANCHI.
 

Similar threads

Dar es Salaam. Sakata la Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma kuendelea kusalia kwenye nafasi hiyo limechukua sura mpya baada ya Wakili wa kujitegemea, Humphrey Simon Malenga kufungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu Masjala Kuu, Dar es Salaam kupinga kiongozi huyo kuongezewa muda wa utumishi huo...
Replies
2
Views
574
Dar es Salaam. Sakata la Profesa Ibrahim Juma kuendelea kuhudumu katika nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania limeibua utata baada ya Jaji wa Mahakama ya Rufani, Stella Mugasha kudaiwa kuandika barua akieleza uamuzi wa kumwongezea muda ni uvunjaji wa Katiba na kutozingatia misingi ya sheria. Hata...
Replies
0
Views
491
Top Bottom